Thursday , 23rd Apr , 2015

Serikali ipo katika hatua za mwisho kuanza ujenzi wa kituo maalum cha kununua na kuuza madini ya vito , ili kuondoa ulanguzi wa madini hayo na kunufaisha serikali.

Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene.

Akizungumza jana katika maonyesho ya kimataifa ya madini ya Vito ya siku tatu, yanayofanyika jijini Arusha, Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, amesema kukamilika kwa kituo hicho kutapandisha mapato ya serikali.

Amesema kuwa kwa sasa Tanzania kupitia maonyesho hayo, inatarajia kupata zaidi ya Sh. Bilioni 3.5, kutokana na ongezeko kubwa la wafanyabiashara wa madini toka nje waliokuja kushiriki maonyesho hayo.

Simbachawene amepongeza maonyesho hayokuweza kuvuta wafanyabiashara wakubwa na wanunuzi wa mataifa mbalimbali duniani na kuitangaza Afrika na rasilimali zake, hivyo anaamini baada ya kukamilika kituo hicho kutadhibiti ulanguzi wa madini na kukomesha utoroshaji wa madini unaofanywa na wajanja wachache.

Aidha amesema katika kituo hicho wataweka uwanja wa kisasa wa kutua na kuruka helkopta mpaka uwanja wa kimataifa wa Kilimanjaro, ili wanunuzi wakinunua tu na kuruka moja kwa moja bila kutumia magari na kujihakikishia usalama wa madini yao.

Pia kutakuwa na hoteli katika kituo hicho ambazo zitalaza wanunuzi wa madini hayo.

Simbachawene ametumia fursa hiyo kupongeza Chama cha Wauza Madini nchini (TAMIDA) na Tanzanite kwa kuweza kufanikisha maonesho hayo na kuwavuta washiriki zaidi ya 700, hali itakayoitangaza Tanzania ipasavyo katika nyanja ya madini.

Aidha amepongeza hatua ya watanzania kuweza kuchonga madini hayo, kwa kuwa kutaongeza soko la ajira kwa vijana na kuachana na kulundikana katika uchimbaji pekee, ambao baadhi yao wanaishia kuwa wasindikizaji na mwisho wa siku hawanufaiki chochote.

Naye Kamishna wa Madini Tanzania, Paulo Masanja, amesema hali ya utoroshaji madini nchini, imepungua, ukilinganisha na mwaka 2013.

Amesema ili kuzuia utoroshaji wa madini machimbo ya Mererani wamejipanga kujenga ukuta, ili kila anayeingia na kutoka aweze kukaguliwa.