Wednesday , 29th Jun , 2016

Serikali kupitia Wizara ya Afya inatarajia kuzindua huduma zote za kiuchunguzi za magonjwa kwenye hospitali ya kisasa ya Benjamin Mkapa iliyopo mjini Dodoma.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii ,Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, wakati alipotembelea hospitali hiyo na kuona inavyoendelea kutoa huduma za afya kwa wananchi.

Waziri Ummy alisema serikali imejipanga katika kutekeleza ahadi yake kwa wananchi katika utoaji huduma bora na za kisasa katika hospitali hiyo.

"Nawaahidi nitafanya uzinduzi rasmi wa huduma za uchunguzi wa magonjwa ili wananchi waelewe hospitali yetu inatoa huduma zipi ili kila mwananchi atambue nini kinapatikana hapa, "alisema Mh. Ummy.

Aidha,Waziri Ummy alisema licha ya kazi nzuri inayofanywa na watoa huduma wa afya wa hospitali hiyo bado inakabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo kukatika kwa umeme mara kwa mara na kuahidi kuwasiliana na wizara ya Nishati na Madini ili kutatua tatizo hilo.

Haha hivyo alisema wizara yake inafuatilia upatikanaji wa fedha kiasi cha shilingi milioni 137 za kukamilisha ujenzi wa ufungaji wa baadhi ya vifaa tiba vilivyopo hospitalini hapo na hivyo kuwakaribisha wananchi wote kufika hospitali hapo kupata huduma za kibingwa za ugonjwa wa kisukari.

Mh. Ummy amesisitiza kuanza kutolewa kwa huduma za vipimo (kama MRI na CT Scan) katika Hospitali hiyo ili kuwapunguzia kero wananchi wa mikoa ya kanda ya kati kupata huduma hizo Dodoma badala ya kusafiri hadi Dar es Salaam kupata huduma hizo.

Hospitali ya Benjamin Mkapa ipo katika Chuo Kikuu cha Dodoma,kwa sasa inahudumia wagonjwa zaidi ya 170 kwa siku,ikikamilika itakua inafanya uchunguzi wa magonjwa ya figo, kisukari pamoja na moyo.