
Dkt. Kigwangalla ameyasema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Jakaya Kikwete aliyeuliza serikali itoe majibu kama wagonjwa waliokuwa wanapata dawa bure kwa mujibu wa sera ya afya hawatapatiwa tena kama lilivyoandika gazeti moja leo likinukuu taarifa toka Muhimbili.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri Dkt. Kigwangalla amesema kwamba gazeti hilo litakuwa limepotosha umma kwani dawa kwa wajawazito, wazee, wagonjwa wa kifua kikuu, ukimwi na watoto wenye umri chini ya miaka mitano watapewa dawa bure katika hospitali za serikali.
Aidha akitoa msisitizo katika swali hilo Waziri wa afya Ummy Mwalimu amesema atawasiliana na hospitali ya Muhimbili ili kujua kwa nini wametoa taarifa isiyo sahihi na baada ya hapo atawasilisha taarifa hiyo Bungeni.