Friday , 13th Feb , 2015

Rais Jakaya Kikwete leo amezindua Sera ya mpya ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ambapo kwa mujibu wa sera hiyo, pamoja na mabadiliko mengine miaka ya kupata elimu ya awali imepunguzwa kutoka miaka miwili hadi mwaka mmoja.

Rais Jakaya Kikwete leo amezindua Sera ya mpya ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ambapo kwa mujibu wa sera hiyo, pamoja na mabadiliko mengine miaka ya kupata elimu ya awali imepunguzwa kutoka miaka miwili hadi mwaka mmoja.

Sera hiyo pia inapunguza umri wa kuanza darasa la kwanza kuwa miaka mitano badala ya miaka saba na muundo wa elimu utakuwa ni 1+6+4+2+3+ badala ya 2+7+4+2+3+ ili mhitimu amalize mzunguko wa masomo kwa muda mfupi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika shule ya sekondari Maji ya Chai iliyoko Kiwalani jijini Dar es salaam, Rais Kikwete amesema kuwa lengo kuu la sera hiyo ni kuifanya Tanzania ifikie lengo lake la kuwa Taifa lenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Rais Kikwete amesema kukua kwa uchumi na ongezeko la watu nchini kumezua changamoto nyingi, hivyo ni lazima elimu inayotolewa ikidhi matatakwa ya mabadiliko huku akiitaka wizara ya elimu kuwa na utaratibu wa kitabu kimoja cha kufundishia kwa kila somo nchi nzima.

Amesema kwamba utaratibu unaotumika sasa kila shule kuwa na kitabu chake cha kufundishia ni chanzo kikuu cha watoto kufeli.

Rais Kikwete pia amezindua maabara za shule za sekondari kitaifa ambapo amesema katika kutambua umuhimu wa elimu nchini bajeti ya wizara ya elimu imeongezeka kwa asilimia 20.

Akizindua maabara kitaifa Rais Kikwete amewataka viongozi ambao hawajakamilisha ujenzi wa maabara katika maeneo yao kuongeza juhudi kwani kipindi cha miezi sita alichoongeza kitaisha akiwa madarakani hivyo hatasita kuchukuwa hatua ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi au kutengua uteuzi.

Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi Mh Shukuru Kawambwa amesema lengo la kuanzisha sera hiyo ni kuhakikisha watoto wa kitanzania wote wanapata elimu bila ubaguzi na kwamba sera imebainisha maeneo ambayo serikali na wadau watayawekea mkazo zaidi ili kutoa elimu bora.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa maabara za shule za sekondari mkoani Dar es Salaam mkuu wa mkoa huo Bw Said Mecky Sadick amesema maabara 281 zenye thamani ya shilingi bilioni 10.9 zimejengwa huku mkuu wa wilaya ya Ilala akitoa taarifa ya ujenzi wa maabara ya kisasa iliyotumika kuzindua maabara zote nchini.