Wednesday , 24th Dec , 2014

Aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi Profesa Anna Tibaijuka amesema licha Rais kumuondoa katika nafasi yake aliyekuwa nayo sasa amerudi jimboni kwake kwa ajili ya kutatua kero na changamoto mbalimbali za wananchi wake.

Aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi Profesa Anna Tibaijuka.

Tibaijuka amesema hayo mkoani Kagera na kuongeza kuwa nafasi aliyokuwanayo ilikuwa haimpi nafasi ya kuwasimamia wananchi katika jimbo lake na kwamba pesa alizopewa na Rugemalila zilikuwa za kusaidia shule na alipewa kama zawadi bila kujua kama pesa hizo zilitoka katika akaunti ya Tegeta Escrow ndo maana hakutaka kujiuzulu mapema.

Nao Wananchi Mkoani Kagera wamepinga uamuzi wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kumuondoa madarakani Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi na kuwaweka kiporo viongozi wengine walioshiriki kuhujumu pesa za akaunti ya Tegeta Escrow.

Wakiongea mkoani humo wamesema hawajajua nini hatima ya Rais kwa kuwaweka kiporo mawaziri wengine waliohusika katika sakata hilo na kumuondoa Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi na pia wamebaki na sintofahamu ambapo wamemtaka Rais kutoa ufafanuzi kuwa licha ya kumg’oa madarakani kiongozi huyo je pesa hizo zitarudishwa kwenye akaunti hiyo ya Tegeta Escrow?.

Nao baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa vya mkoa huo akiwemo Katibu wa siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera Hamimu Mahamudu amepongeza uamuzi wa Rais alioutoa wakati akiongea na wazee wa mkoa wa Dar es salaam kwa kumuondoa kiongozi huku Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, katika manispaa ya Bukoba Victor Sherejei akisema kuwa Rais hajatoa uamuzi sahihi ambapo amemtaka Rais kuwafahamisha watanzania kuwa pesa za Escrow zitarudishwa lini katika akaunti hiyo au kuwaondoa viongozi madarakani ndiyo suluhisho la kwamba pesa hizo hazirudishi.