Wednesday , 24th Oct , 2018

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mh. Gelasius Byakanwa amefanikiwa kuuzima moto wa wafanyabiashara mjini Mtwara kufuatia mgomo wa kufungua maduka asubuhi ya leo wakilalamikia tozo kubwa ya ushuru iliyopandishwa na halmashauri ya manispaa hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa www.eatv.tv, Mh. Byakanwa amesema kuwa alipopata taarifa hizo alikwenda eneo la tukio kuwasikiliza, na kutafuta suluhu ya tatizo hilo ambalo waathirika wakubwa ni wananchi.

"Nimetoka hapo sasa hivi, wafanyabisahara nimeongea nao, nimemuita Mkurugenzi na mheshimiwa Mkuu wa Wilaya nimeacha wawasikilize wafanyabiashara hao malalamiko yao, lakini wakati huo huo huduma ziendelee kwa wananchi, nilichokitaka ni uongozi wa wafanyabiashara ukutane na Mstahiki Meya pamoja na Mkurugenzi, na wafanye kikao ambacho kitatoa majibu ya kero za wafanyabiashar”, amesema Mh. Byakanwa.

Leo asubuhi wafanya biashara wa soko kuu mjini Mtwara waligoma kufungua maduka wakilalamikia tozo kubwa ya ushuru iliyoongezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani,  inayowataka kulipa shilingi elfu 75 kwa kila jengo badala ya elfu 25 iliyokuwa hapo awali.