Wednesday , 28th Sep , 2016

Rais Dkt. John Magufuli leo amezindua ndege mbili mpya zilizonunuliwa na serikali nchini Canada aina ya Bombardier Q400 ambazo zina uwezo wa kubeba watu 76 pamoja na mizigo kwa wakati mmoja.

Rais Magufuli, Mkewe Mama Janeth Magufuli na baadhi ya maafisa wa serikali katika moja ya ndege zilizozinduliwa leo

Akizungumza katika uzinduzi huo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl. Nyerere Jijini Dar es salaam, Rais Dkt. Magufuli ametumia muda huo kuwataka wafanyakazi wa shirika la ndege nchini kutubu kutokana na dhambi ambazo zimekuwa zikifanywa na shirika hilo kuanzia viongozi hadi wafanyakazi wa kawaida.

“Baadhi ya dhambi zilizokuwepo ATCL ni pamoja na kutokuwa na mfumo wa kujiendesha na kutegemea kila kitu kutoka serikalini, viongozi kujilipa posho zisizo na maslahi kwa shirika na kwa watanzania, wafanyakazi kufanya vitendo vya kulihujumu shirika, kutofuata ratiba kulingana na tiketi zilivyokatwa” Amesema Rais Dkt. Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amesema kuwa katika shirika hilo kulikuwepo na mafuta hewa ambapo ilikuwa ikiandikiwa mafuta ya kwenda Mwanza wakati haijaenda, na mafuta yanahesabika kuwa yametumika jambo ambalo liliongeza gharama za shirika hilo.

Pamoja na hayo Rais Dkt,. John Magufuli amemtaka Mkurugenzi Mpya wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi kufanya kazi na wafanyakazi wenye kasi inayotakiwa kwa sasa na ambao hawatafanya hivyo waondolewe mara moja.

“Tuliweza kufukuza wafanyakazi 500 wa NIDA hatutashindwa kufukuza 200 wa ATCL, kuna vijana wengi wapo mtaani wanatafuta kazi , maana wengi hapa wamezoea kufanya kazi kwa mazoea” Amesema Rais Dkt. Magufuli.

Ndege zilizozinduliwa leo zitakuwa zinafanya kazi katika viwanja 12 nchini na pia zina uwezo wa kwenda nchi jirani ambapo zina uwezo wa kutua katika viwanja ambavyo vina lami au rafu katika njia zake za kutua.