Monday , 31st Oct , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo ameondoka nchini kuelekea Nairobi nchini Kenya kwa ziara ya Kiserikali ya siku mbili nchini humo kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta.Mhe. Uhuru Kenyatta.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Rais Magufuli ameagwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Mkuu wa Mkoa wa Dar Es salaam, Paul Makonda na viongozi mbalimbali wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiagana  na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa  tayari kwa safari ya kwenda Nairobi, Kenya kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili  Oktoba 31, 2016

 

Mara baada ya kuwasili nchini Kenya, Rais Magufuli atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, na baadaye atakwenda kutoa heshima katika Kaburi la Rais wa Kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta.

Pamoja na kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais Magufuli atakwenda kutoa heshima katika Kaburi la Rais wa Kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta na pia anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa aliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta Ikulu Jijini Nairobi

Katika ziara hii Rais Magufuli anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha Eldoville kilichopo Karen Jijini Nairobi, na pia anatarajiwa kuzindua barabara mchepuko ya Southern By-pass iliyopo Jijini Nairobi.

Southern By-pass

Barabara hiyo mchepuko ya Southern By-pass ni moja kati ya miradi mikubwa ya barabara nchini Kenya, inaunganisha maeneo mbalimbali ya Jiji la Nairobi kwa barabara za juu na chini na imejengwa kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika Jiji hilo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akipunga mkono wakati akipanda ndege kwenye  Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tayari kwa safari ya kwenda Nairobi, Kenya kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili Oktoba 31, 2016 

 

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda na viongozi wengine wakipunga mikono kumuaga Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakati akianza safari ya kwenda Nairobi, Kenya kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili Oktoba 31, 2016