Saturday , 1st Aug , 2015

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt, Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani ambayo kitaifa inatarajiwa kufanyika mkoani Tanga.

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt, Jakaya Mrisho Kikwete.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Magalula Saidi Magalula amesema Rais kikwete atawasili jijini Tanga siku ya jumapili na kufanya uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani siku ya tarehe tatu mwezi wa nane katika viwanja vya tangamano jijini hapa.

Magalula amesema katika maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani kutakuwa na mambo mbalimbali ikiwemo fursa ya kupima afya kwa madereva wa vyombo vya moto, mafunzo maalum kwa waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda, mafunzo kwa walimu wa shule za msingi ili kuweza kuwaelimisha wanafunzi pindi watakaporudi mashuleni mwao.

Wiki ya nenda kwa usalama barabarani inatarajiwa kuanza tarehe tatu mwezi wa nane na kufikia kilele tarehe saba mwezi wa nane ikiwa kauli mbiu ya mwaka huu ikisema ENDESHA SALAMA OKOA MAISHA.

Sambamba na hayo Magalula ameongeza kuwa Rais kikwete pia, atatumia muda wake kuzungumza na wakazi wa jiji la Tanga nyakati za jioni katika uwanja wa Mkwakwani kwa lengo la kuwaaga rasmi wakazi wa Tanga na kuwashukuru katika kipindi chake chote alichokuwa kwenye uongozi.