Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, jana, Alhamisi, Agosti 21, 2014, ameweka historia nyingine katika ziara yake ya Mkoa wa Morogoro wakati aliposafiri kwa treni ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), ikiwa ni mara yake ya kwanza kutumia usafiri huo katika kipindi chake cha Urais.
Rais Kikwete, akifuatana na Mama Salma Kikwete, amesafiri kilomita 143 ndani ya Behewa la Kirais (Presidential Coach) la T-One kwa kiasi cha saa tatu na dakika 25 akitokea stesheni ya Ifakara katika Wilaya ya Kilombero kwenda Stesheni ya Kisaki, Wilaya ya Morogoro.
Rais Kikwete akiandamana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Joel Bendera na Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, amepanda treni hiyo kiasi cha saa 4:45 asubuhi mjini Ifakara na kushuka 8:10 mchana wakati alipowasili Kisaki. Kwa muda mwingi alikuwa katika Chumba cha Mikutano (Conference Room) cha Behewa la Kirais hilo ambalo pia lina huduma nyingine nyingi za Kirais.
Rais Kikwete anakuwa Rais wa tatu wa Tanzania kutumia Behewa hilo na kusafiri ndani ya treni ya TAZARA. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye TAZARA ilibuniwa na kujengwa chini ya uongozi wake, alitumia Behewa hilo na treni hiyo mara mbili, mara ya kwanza ikiwa mwaka 1976 aliposafiri na mgeni wake, aliyekuwa Rais wa Sierra Leone, Mheshimiwa Siaka Stevens.
Rais wa Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi pia alitumia Behewa hilo na usafiri wa TAZARA mara mbili wakati Rais wa Tatu, Mheshimiwa William Mkapa hakupata kutumia Behewa hilo wala usafiri wa TAZARA.
Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Rais Kikwete kuweka historia katika ziara yake ya siku saba katika Mkoa wa Morogoro iliyoanza jana, Jumatano, Agosti 20, 2014.
Katika siku yake ya kwanza jana, msafara wa Rais Kikwete, uliweka historia kwa kuwa magari ya kwanza kuvuka Mto Kilombero kwa kutumia daraja, ukiwa unatokea Wilaya ya Ulanga kuingia Wilaya ya Ifaraka ambako Rais aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja kamili kwenye Mto huo.
Msafara huo, ulivuka Mto huo kwa kutumia daraja jembamba la chuma ambalo linatumiwa kama daraja la muda na mafundi wa Kampuni ya Kichina ambayo inajenga daraja kubwa na la kweli kweli kwenye Mto huo linalogharimu Sh. bilioni 56 zinazotolewa na Serikali ya Tanzania.
Kutokana na adha ya karne na karne ambayo wananchi wa wilaya hizo mbili wamekuwa wanaipata kuvuka Mto Kilombero kwa kivuko na hata mitumbwi, wananchi wa maeneo hayo wamelipachika Daraja hilo jina la Daraja la Ukombozi.
Daraja la Mto Kilombero ni moja ya madaraja makubwa matatu ambayo Rais Kikwete, katika kampeni yake ya Urais ya mwaka 2005, aliahidi kuyajenga na ambayo yaliwekwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Madaraja mengine ni lile la Kigamboni, Dar Es Salaam, ambalo ujenzi wake unaendelea na Daraja la Mto Malagarasi Mkoani Kigoma ambalo ujenzi wake umekamilika.
Madaraja hayo matatu, na mengine mawili, ya Kirumi kwenye Mto Mara na la Rufiji ni madaraja ambalo yalikuwa yamepangwa kujengwa katika Mpango wa Kwanza wa Taifa wa Maendeleo. Daraja la Kirumi lilijengwa wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere na lile la Rufiji lilijengwa wakati wa uongozi wa Mzee Mkapa. Matatu yaliyobakiwa yamejengwa wakati wa Uongozi wa Rais Kikwete.