Saturday , 13th Feb , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa agizo la siku mbili kwa hospitali ya Taifa Muhimbili kuhakikisha wazazi wahamie katika jengo la ofisi na watu wa ofisini watafute sehemu nyingine.

Rais amesema alikasirishwa sana alipotembelea hospitali hiyo na kukuta wakina mama wamelala sakafuni chini huku uongozi wa hospitali hiyo ukiwa umekaa kimya juu ya tatizo hilo.

''Nilipofika pale kina mama wakaniita kwenye wodi yao wasaidizi wangu wakaniambia nisiende nikawaambia huku huku ndiko ninakoenda kwenda nilikuta mambo ya hovyo sana kina mama wanalala wanne mpaka watano, niliahidi kufanyia kazi jambo hilo'' Amesema Rais.

''Sasa naagiza kina mama hao wapewe jengo la ofisi na vitanda vifungwe na wahamishiwe kwenye jengo hilo ndani ya siku mbili'' Amesisitiza Rais Magufuli.

Pia Rais ameshangazwa katika hospitali hiyo kuwa na jengo la ghorofa tatu ambalo halijakamilika kuanzia uongozi wa Rais Mwinyi hadi sasa na viongozi wapo wakishindwa kuchukua hatua na kuagiza mamlaka za chini yake kuhakikisha zinachukua hatua.

Rais Magufuli amefanya uamuzi huo leo wakati akizungumza na wazee wa jiji la Dar es salaam ambapo pamoja na mambo mengine amewataka watanzania kufanya kazi kwa bidii na kuiombea serikali yake ili itimize yote iliyoahidi kwa watanzania.