Mhe. Rais Magufuli amewataka wakurugenzi waliokula viapo vya utumishi kusimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato ya serikali na ametumia nafasi hiyo kuagiza wizara zote kuanza kutumia mashine za kielektroniki (EFD) katika ukusanyaji wa mapato kwenye taasisi zote ambazo zinakusanya maduhuli.
Dkt. Magufuli amewasisitiza wakurugenzi hao kuhakikisha wanasimamia vizuri fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya utoaji wa elimu ya msingi na sekondari bila malipo, ambapo kila mwezi serikali hutoa shilingi bilioni 18.777 na ametaka tabia ya wakurugenzi wa halmashauri kushirikiana na wafanyabiashara ama wanasiasa kujinufaisha kupitia zabuni za serikali ikome.
kwa upande wao Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ambao walikuwepo wamewataka wakurugenzi hao wa halmashauri kuwa watumishi bora, kusimamia vizuri rasilimali za halmashauri na kushirikiana na viongozi wa mkoa na wilaya katika halmashauri zao.



