Thursday , 21st Aug , 2014

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetangaza kuanza operesheni ya kusambaratisha mitandao inayotumika kuratibu mauwaji ya watu wenye albinism ikiwa ni siku chache baada ya kuripotiwa kuongezeka kwa matukio hayo nchini.

Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini Tanzania DCI Issaya Mngulu.

Akiongea leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI Isaya Mngulu amesema jeshi la polisi limeamua kutangaza operesheni hiyo kufuatia matukio matatu yaliyotokea mwaka huu katika mikoa ya Simiyu pamoja na mkoa wa Tabora.

DCI Mungulu amesema wananchi waendelee kutoa taarifa ili kufanikisha operesheni hiyo, huku akizitaka taasisi za kidini, asasi za kiraia, wanasiasa pamoja na wazee wa kimila kuendelea kuielimisha jamii ili kuachana na imani za kishirikina zinazochochea mauaji hayo.

Kauli hiyo ya polisi imekuja baada ya watu wenye albino hapo jana kueleza kuwa kuendelea kushamiri kwa vitendo vya ukatili na mauaji dhidi ya watu wenye albinism, kunachangiwa mno na kuogopwa kwa viongozi wa kichifu na waganga wa jadi katika maeneo mengi yanapotokea matukio hayo.

Meneja Uendeshaji kutoka shirika la Under The Same Sun, Bw. Jamali Limboya alisema kuwa vyombo vya dola na wananchi wengi wanahofia usalama wa maisha yao kutokana na kuogopa uwezo wa kishirikina walionao watu hao.

Maye Mtoto Mariam Stamford ambaye ni mlemavu wa ngozi aliyefanyiwa ukatili wa kukatwa mikono yake miwili amemuomba Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati kukomesha kabisa tatizo la ukatili na mauaji wanaofanyiwa watu wenye albinism nchini Tanzania.

Akiongea kwa masikitiko leo kwenye mahojiano yaliyofanyika kwenye kipindi cha Supa Mix cha East Africa Radio, Mariam amesema iwapo wanyama pori wanawekewa ulinzi wasiuwawe na majangili, iweje ishindikane kwa watu wenye albinism.