Tuesday , 14th Jun , 2016

Kongamano la chama cha ACT wazalendo limeshindwa kufanyika hii leo baada ya Jeshi la Polisi Kushikilia msimamo wa kulizuia Kongamano hilo kwa madai kuwa linalenga kuchochea uvunjifu wa amani.

Taarifa iliyotolewa na chama hicho kwa waandishi wa habari hii leo jijini Dar es salaam baada ya kuahirisha kongamano lake la kujadili bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho ndugu Ado Shaibu amesema wanakitafsiri kitendo hicho kama mbinu ya kuzima mjadala wa bajeti na kuminya demokrasia.

Ado Shaibu amesema, katika mahojiano na polisi na kiongozi wa chama hicho ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini Mhe. Kabwe Zitto, amesema Polisi walihoji zaidi kuhusiana na kongamano hilo ambalo ACT imedai kuwa ni haki ya kisheria ya vyama vya siasa.

Ado pia amesema wanasheria wa chama hicho wapo kwenye hatua za ku shughulikia kufungua kesi ya kikatiba kupata tafsiri ya kimahakama dhidi ya vitendo hivi vya jeshi la polisi kuzuia mikutano ya hadhara na makongamano ambayo ni haki ya kisheria ya vyama vya siasa.