Thursday , 25th Oct , 2018

Siku moja baada ya Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba kudai kuwa maelezo ya polisi kuhusu ajali iliyosababisha vifo vya watumishi watano wa wizara hiyo hayakuwa ya kweli, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, amesema hayupo tayari kufafanua lolote kuhusu madai ya waziri huyo.

Kamanda wa  Polisi Singida, Sweetbert Njewike.

Kupitia kipindi cha 'East Africa Breakfast', cha East Africa Radio, iliyomtafuta Kamanda wa  Polisi Singida, Sweetbert Njewike ili kutoa ufafanuzi wa madai hayo ya waziri, alidai kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo.

"Suala hilo siwezi kulizungumzia kabisa, hapana", amesema Kamanda na kukata simu.

Ajali hiyo ilitokea Jumapili iliyopita katika kijiji cha Njirii, Manyoni mkoani Singida na kusababisha vifo vya watumishi wa serikali waliokuwa katika gari namba STK 8925, iliyogongana uso kwa uso na lori, ambapo taarifa ya Kamanda wa Polisi ilieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi ambapo dereva wa gari la serikali alijaribu kuyapita magari bila tahadhari na hatimaye kugongana na lori hilo.

Hata hivyo Waziri Tizeba akiwa katika viwanja vya wizara hiyo jijini Dar es salaam, Jumatatu ya wiki hii alisema taarifa iliyotolewa na polisi si ya kweli na kwamba jeshi hilo linapaswa kwenda eneo la tukio na kujiridhisha tena, Dk. Tizeba aliongeza kuwa dereva wa gari hilo ni mzoefu wa kuendesha magari na kwamba asingeweza kufanya uzembe unaotajwa kufanyika.