Sunday , 5th Jun , 2016

Majambazi watatu wameuwa katika majibizano ya risasi na askari polisi alfajiri ya kuamkia leo katika mapango ya mlima wa Utemini wilayani Nyamagana mkoani Mwanza..

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Ahmed Msangi

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Ahmed Msangi imesema kuwa siku ya ijumaa askari polisi,walifanikiwa kumkamata Omary Francis Kitaleti Kiberiti, baada ya kupewa taarifa mtu huyo kuhusika katika matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha kwenye maduka ya kutolea huduma za hela kwa njia ya Mtandao.

Kamanda Msangi amesema baada mtuhumiwa huyo kuhojiwa alikiri kuhusika katika matukio hayo na aliwataja wenzake wanaoshirikiana nao na mahali walipojificha na kwenda kuonyesha maficho ya wenzake yaliyokuwepo kwenye mapango ya mlima wa Utemini kata ya Mkolani wilayani Nyamagana.

Kamanda Msangi ameeleza kuwa Polisi walifika katika mlima huo ghafla walianza kushambuliwa kwa risasi na majambazi waliokuwa wamejificha ndani ya mapango hayo na katika majibizano hayo risasi ziliweza kumpata jambazi aliyekuwa anawaongoza askari polisi na kufariki dunia papo hapo, na risasi nyingine ilimjeruhi askari kwenye unyayo wa mguu wa kulia.

Katika majibizano ya risasi na majambazi hayo kwenye mapango askari polisi walifanikiwa kumuua jambazi mmoja ambaye hajafahamika jina na wengine walifanikiwa kukimbia ambapo Afajiri walifanikiwa kumpata mmoja ambae aliuawa huku wingine watatu wakifanikiwa kukimbia na jeshi la Polisi linaendelea na msako dhidi ya watu hao.