Friday , 6th Feb , 2015

JESHI la polisi mkoa wa Mara limefanikiwa kukamata bunduki mbili aina SMG, Risasi 427 pamoja na Magazine nane katika vijiji viwili wilayani Serengeti mkoani humo.

Bunduki na risasi zilizokamatwa

JESHI la polisi mkoa wa Mara limefanikiwa kukamata bunduki mbili aina SMG, Risasi 427 pamoja na Magazine nane katika vijiji viwili wilayani Serengeti mkoani humo ambazo zilikuwa zikitumika katika matukio ya uwindaji haramu wa Tembo katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mara, kamishina msaidizi wa jeshi la polisi ACP Philip Alex Kalangi,amewaambia waandishi wa habari mjini Musoma kuwa bunduki ya kwanza na risasi 176 pamoja na magazine nne imekamatwa eneo la kijiji cha Bochugu wilayani Serengeti baada ya watu wanadaiwa kuwa majangili kuingia katika hifadhi hiyo kwa lengo la kuua tembo lakini kabla ya kufanya uwindaji huo haramu walikurupushwa na askari wa hifadhi ya tanapa kisha kutelekeza sihala na risasi hizo.

Katika tukio la pili kamanda huyo wa polisi mkoa wa Mara amesema kuwa Mwanamke mmoja Bi Christina Magige mkazi wa kijiji cha Mbilikiri wilayani Serengeti amesalimisha Silaha moja aina ya SMG, risasi 251 na magazine nne ambayo inadaiwa kutumiwa na mme wake Bw Machori Mwita kwa ajili ya uhalifu ukiwemo uwindaji haramu wa tembo katika hifadhi ya taifa ya Serengeti.

Kamanda Kalangi amesema katika Operesheni hiyo inayoendelea mkoani Mara, pia jeshi la polisi limefanikiwa kakamata Bangi kavu ambayo ilikuwa imehifadhiwa katika mifuko minne ya kilo 50 kila mmoja katika kijiji cha Bukabwa wilayani Butiama pamoja na meno mawili ya tembo katika kijiji cha kisangura wilayani Serengeti.