
Jeshi la Polisi nchini kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, limesema kuwa limejipanga vizuri kudhibiti vitendo vya uhalifu vitakavyojitokeza hususani katika kipindi hiki cha kuelekea mkesha wa mwaka mpya.
Taarifa iliyotolewa leo na msemaji wa jeshi hilo Advera Bulimba imesema kuwa ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.
Pia, jeshi hilo limewatahadharisha watu wote ambao watakuwa wakitumia barabara kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani na hasa kwa madereva wa magari na pikipiki, kuepuka kujaza watu kupita kiasi, kwenda mwendo kasi, kutumia vilevi pamoja na kupiga honi hovyo.
Vilevile limewataka wananchi kuacha tabia ya kuchoma matairi barabani pamoja na kupiga mafataki.
Aidha, Jeshi la Polisi limetoa tahadhari kwa wananchi wote kuwa makini na kuchukua hatua stahiki za haraka kwa kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo yao ya makazi ama maeneo ya biashara.
Amesema yeyote atakayefanya vitendo hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Bulimba ametaja namba za simu za polisi endapo mwananchi atakuwa na taarifa kuwa ni ni 111 au 112