Monday , 9th Feb , 2015

Wakulima wa kahawa mkoani Kilimanjaro wamepata hasara kubwa msimu huu wa kilimo kutokana na wengi wao kutumia pembejeo feki zinazosambazwa na wafanyabiashara wasio waaminifu.

Hayo yamebainishwa na mshauri wa chama cha wanawake wahamasishaji kilimo cha kahawa Tanzania (TAWOCA) Bw. Zebedayo Swai na kusema kuwa hali hiyo imezidi kukatisha tamaa wakulima wa kahawa.

Amesema ni vema serikali ikangalia uwezekano wa kudhibiti uingizwaji wa pembejeo za kilimo feki ambazo zimekuwa zikiingizwa kila mwaka hapa nchini na kusababisha wakulima kupata hasara licha ya kuuzwa kwa bei ghali.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha wanawake wahamasishaji kilimo cha kahawa Tanzania (TAWOCA) Bi Fatma Faraja amewataka wanawake kujihusisha na uzalishaji wa kahawa bora ili kujiimarisha kiuchumi na kuachana na dhana potofu ya kuwa kahawa ni kwa ajili ya wanaume.

Naye afisa masoko wa chama kikuu cha ushirika mkoani kilimanjaro (KNCU) Bi. Sia Makishe amesema tatizo hilo limesababisha udhalilishaji wa kahawa mkoani Kilimanjaro kushuka na hivyo kushindwa kufikia makisio waliojiwekea.