Waziri wa uchukuzi nchini Tanzania Dkt Harrison Mwakyembe.
Serikali ya Tanzania imewasimamisha kazi maafisa 13 wakaguzi katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JK Nyerere kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa wageni katika uwanja huo.
Akizungumza leo Jijini Dar-es-Salaam Waziri wa Wizara ya Uchukuzi Dk. Harisson Mwakyembe amewataka maafisa hao kuondoka uwanjani hapo ambapo ametaja wizara wanazotoka kuwa ni Kilimo, Afya na Mifugo.
Dkt. Mwakyembe katika kudhibiti suala hilo kutojirudia ameutaka uongozi wa uwanja huo kuhakikisha kuwa kila afisa anavaa sare pamoja na uwepo ufuatiliaji wa kina wa nyendo zao.
Wakati huohuo, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini Tanzania imesisitiza kuwepo katika mkakati wa kuwanyima viza za kwenda nje ya nchi wanafunzi wanaopanga kwenda kusoma au kufanya kazi iwapo wanadaiwa na bodi hiyo, mpaka pale watakapofuata utaratibu wa kuirejesha mikopo hiyo .
Akizungumza na EATV, Mkurugenzi wa Habari wa bodi hiyo Cosmas Mwaisoba amesema wamechukua hatua hiyo baada ya kuonekana kuwa kuna ujanja unatumika kukwepa urejeshwaji wa mikopo hiyo.
Aidha, ameongeza kuwa bodi ipo katika mkakati wa kuwafikia wale wote wanaodaiwa mikopo ambao wapo nje na ndani ya nchi na wamepitisha muda wa kulipa mikopo yao.