Monday , 13th Apr , 2015

Zoezi la uandikishaji wa wananchi katika daftari la kudumu la mpiga kura kwa mfumo wa kielektroniki (BVR) limeingia katika hatua ya mwisho mkoani Njombe tangu kuzinduliwa Februari 24 katika halmashauri ya mji wa makambako.

Wasimamizi wa uandikishaji wa Daftari la kudumu la Mpiga kura wakiwa tayari kwa ajili ya zoezi hilo.

Uandikishwaji huo unatarajia kumalizika April 15 na kwamba kata zilizo salia kila halmashauri zimeanza kukamilisha uandikishaji kwa kata za kuhitimisha lilianza Aprili 9 ambapo katiaka halmashauri ya mji wa Njombe kata za Ramadhani na Njombe mjini zilizowekwa kiporo zimeanza uandikishaji.

Kituo hiki kimepita katika vituo mbalimbali ndani ya kata za Njombe Mjini na Ramadhani hususani vituo vilivyopo mitaa ya Kibena na Idundilanga na kujionea foleni ndefu ambayo bado imeendelea kuzua malalamiko kwa baadhi ya wakazi ambao wanaiomba tume kubadili ratiba ya kufungua vituo kwani wamekuwa wakifika usiku kujiandikisha huku vituo vikifunguliwa saa mbili kama ilivyopangwa

Lameck Ulaya ni mwenyekiti wa Mtaa wa Idundilanga Ambao una Jumla ya vituo vinne ya Kuandikisha na ambaye Amesema huenda Wananchi wakawa na dhamira ya dhati katika kuwapata viongozi wao katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba kutokana na mwamko mkubwa wa jamii kujitokeza katika vituo vyao pamoja na kuhimiza wananchi wengi kuendelea kujitokeza

Zoezi hilo katika kata za Njombe mjini linaonekana kuwa na mafanikio makubwa kutokana na tume kuamua kuwatumia waandikishaji kutoka kata nyingine na hivyo wana uzoefu na mashine za BVR ambapo zaidi ya watu 150 katika vituo kwa kila kituo kwa siku moja.