Monday , 18th Jul , 2016

Mwenyekiti wa TLP Dkt. Augustino Mrema amesema kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole ni kutokana na uzoefu wake serikalini na siyo kumlipa fadhila.

Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Agustino Mrema

Mrema ameyasema hayo alipofanya mazungumzo na EATV kuhusu uwezo wake wa kuitendea haki nafasi aliyoaminiwa na Rais Dkt. John Magufuli.

‘’Rais ana washauri wake kabla hajaamua jambo,. Wala siyo kwamba kanilipa fadhila , mimi nina utumishi uliotukuka serikalini , nimekuwa Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi nimekuwa Waziri wa Vijana na maendeleo ya vijana, nimekuwa Naibu Waziri Mkuu wa Serikali nani asiyejua hilo uzoefu wangu kwenye eneo hilo upo wazi hasa kipindi cha Rais Mwinyi nani asiyejua hilo’’ Amesema Dkt. Mrema

‘’Lengo la kuniteua haina maana ya kuuwa upinzani na kuwa upinzani siyo kwamba kususia kila kitu, leo amepatikana mtu ambaye anafanya kazi kubwa kwa nini tusimuunge mkono, na kama ingekuwa fadhila wananchi wa Vunjo wangenichagua kwa kuwa aliwaambia wanipigie kura na hawakunipigia’’ameongeza Dkt. Mrema.

Aidha Dkt. Mrema amesema atazunguka katika magereza mbalimbali nchini ili kuenda kuwaelimisha umuhimu wa parole na kama wakitulia magerezani kwa kufuata sheria atashirikiana na wenzake kuwatoa wawe nje na kupangiwa kazi maalumu za kijamiii na kupewa namna ya kuwasimamia.

Kuhusu uzee Mrema amesema ana miaka 72 tu na haoni kama ana uzee unaomshinda kufanya kazi hiyo hivyo anawahakikishia wananchi kwamba ana uwezo wa kufanya kazi hiyo kwa uadilifu na ari kubwa.