Wednesday , 18th Nov , 2015

TUME ya Taifa ya Uchaguzi ( NEC) imesema hadi sasa viti maalumu vya Udiwani ambavyo madiwani wake

Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC Dk. Ramadhani Kailima, Kulia Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sheria NEC Bw. Emanuel Kawishe Wakizungumza na waandishi wa Habari hawapo pichani.

TUME ya Taifa ya Uchaguzi ( NEC) imesema hadi sasa viti maalumu vya Udiwani ambavyo madiwani wake wameteuliwa na tume hiyo ni viti 1393, kutoka katika Vyama vya CCM, CHADEMA, NCCR- MAGEUZI pamoja na CUF.

Hayo yamesemwa jijijini Dar es Salaam na mkurugenzi wa uchaguzi kutoka NEC Bw. Kailima Ramadhani wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu uteuzi wa madiwani wanawake wa viti maalumu.

Aidha Bw.Ramadhani amesema kuwa idadi ya viti maalum vya udiwani ni 1,408 na kwamba kutokana na majimbo nane na kata thelathini na Nne ambapo uchaguzi haujakamilika kwa sababu mbalimbali, hatua hiyo itasababisha kubakia viti 15 ambavyo vitagawanywa mara baada ya uchaguzi kukamilika ili kufikia idadi ya viti 1,408 kutoka viti 1393 vinavyo tambulika kwa sasa.

Aidha amefafanua kuwa kutokana na viti hivyo maalumu vya udiwani vilivyoteuliwa na NEC, Chama Cha Mapinduzi CCM kimepata viti 1,022,Chama Cha Demokrasia na Mawendeleo CHADEMA 280, Chama Cha Wananchi CUF-79, ACT WAZALENDO viti 6 pamoja na NCCR MAGEUZI viti 6.

Alisema kuwa tume imeamua kutoa taarifa ya uteuzi wa viti maalumu vya udiwani nchi nzima ya madiwani walioteuliwa na tume kutokana na Kanuni za Kudumu za Mikutano ya Halmashauri, Mabaraza ya Madiwani yanatakiwa kuitishwa siku thelathini tangu tarehe ya Uchaguzi ifanyike.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi NEC alisema kuwa mwisho wa uchaguzi katika majimbo na kata ambazo hazikufanya uchaguzi ni Desemba 20 mwaka huu, ambapo katika jimbo la Ulanga Mashariki pamoja na Lushoto uchaguzi utafanyika Novemba 22 mwaka huu, na kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuchagua kiongozi wanayemtaka.

Hata hivyo ,Bw. Ramadhani Kailima imevitaka vyama vya siasa vilivyoshindwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba mwaka huu kukubali matokeo ya uchaguzi huo ambapo alisema wakati wa uchaguzi kulikuwa na fomu maalum ambazo mawakala walisaini kukubaliana na matokeo katika vituo vya kupigia kura pamoja na kujumlishia kura ambazo ndio vielelezo vya ushahidi wa matokeo.

Bw. Kailima alisema wagombea wajenge utamaduni wa kukubaliana na matokeo hata kama wameshindwa kutokana na mchakato wa uchaguzi kuzingatia misingi yote kuanzia ngazi ya Udiwani, Ubunge mpaka Urais.