Mkurugenzi wa masuala ya Sheria wa NEC, Bw Emmanuel Kawishe
Akiongea na East Africa radio Mkurugenzi wa masuala ya Sheria wa NEC, Bw Emmanuel Kawishe amesema kuwa ugawaji wa vituo vya kupigia kura umefuata sheria na vituo vimegawanywa kwa vipengele ili kurahisisha upigaji kura kwa wananchi na hakuna kituo chochote kilichoongezeka.
Aidha Bw, Kawishe ameongeza kuwa viongozi waache kuwadanganya wananchi kuhusu karatasi za kupigia kura kuwa zinahamisha alama za mgombea na kusema kabla ya kupeleka vituoni vyama vyote vinahakiki karatasi hizo huku akiwataka wananchi kufuata sheria ya kutokuweka mikusanyiko mara ya kupiga kura kama wanavyoelekezwa na viongozi wa vyama vyao.
Kawishe amesema kuwa kwa mujibu wa sheria kila chama kinatakiwa kuweka wakala ndani ya chumba cha upigaji kura na ndio mwenye jukumu la kuhesabu kura, hivyo kuweka mikusanyiko isiyokuwa na kibali ni kuhatarisha amani kwa kuwa ni kinyume cha sheria.
Amesema tume inaendesha mchakato wa uchaguzi mkuu kwa mujibu wa sheria kama ilivyofanya miaka ya nyuma na itatangaza matokeo kwa utaratibu ule ule ambao utaondoka kero na sintofahamu kwa vyama na wananchi kwa ujumla.