Mwenyekiti wa NEC, Jaji Kaijage.
Akisoma taarifa iliyotolewa kwa wanahabari, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Semistocles Kaijage leo Aprili 4, 2019 jijini Dar es salaam, amesema kuwa uchaguzi huo utafanyika tarehe 19 Mei mwaka huu, huku fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kati ya tarehe 15 hadi tarehe 19, Aprili.
Aidha Jaji Kaijage amesema kwamba kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 20, Aprili hadi tarehe 18 Mei mwaka huu ambapo uchaguzi huo utafanyika sambamba na Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki.
“Tume inapenda kuvikumbusha Vyama vya Siasa na wadau wote wa Uchaguzi kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na Maelekezo yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi chote cha Uchaguzi huu mdogo,” amesema Jaji Kaijage.
Jaji Kaijage amesema kuwa maamuzi ya kutangaza uchaguzi kwenye kata hizo yamefanyika baada ya Tume kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa ambaye kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 aliitaarifu Tume juu ya uwepo wa nafasi hizo.
Kata hizo ni pamoja na Uwanja wa Ndege iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi, Kitobo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera, Kyela iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya, Mikocheni iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam, Mvuleni iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Mkoani Lindi na Manda iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.





