Friday , 20th Feb , 2015

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania - NEC, imesisitiza kuwa zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura lipo pale pale na kwamba zoezi hilo litaanza jumatatu ya wiki ijayo kama ilivyopangwa hapo awali.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva.

Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Damian Lubuva, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na maofisa pamoja na waratibu wa zoezi la uboreshaji wa daftari hilo, linalotarajia kuanza mkoani Njombe siku hiyo ya Jumatatu.

Jaji Lubuva amesema tume yake inaendelea na taratibu za kufanyika kwa uboreshaji huo, na kuwaonya wanasiasa kujiepusha na kile alichokiita kuwa ni ukiukwaji wa sheria, kutokana na kuwepo kwa taarifa kuwa baadhi yao wamekuwa wakiwashawishi wananchi wafanye fujo na kukataa kushiriki katika zoezi hilo.

Wakati huo huo, Mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji nchini Tanzania – EWURA, imekubali ombi la shirika la maendeleo ya mafuta nchini TPDC, la tozo za gharama za huduma za kuchakata na kusafirisha gesi asilia kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara kuja jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Bw. Felix Ngamlagosi amesema EWURA imeridhia maombi hayo ya TPDC baada ya kupata maoni kutoka pande zote za wadau wa gesi nchini, ikiwa ni pamoja na watumiaji pamoja na Baraza la Kutetea Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji yaani Consumer Consultative Council.

Ngamlagosi amesema baada ya kupitia maoni ya wadau pamoja na kufanya hesabu za kitaalamu kuhusu suala hilo, EWURA imeridhia kupitisha dola 2.14, zaidi ya fedha za Tanzania shilingi 3800, kati ya dola za Marekani 4.178 zilizoombwa na TPDC kwa ajili ya kugharamia huduma twajwa hapo juu.