Agizo hilo limetolewa leo na Waziri wa Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma kuhusiana na sababu zilizolilazimu Baraza la mitihani nchini (NECTA) kubadili mfumo wa matokeo ya mitihani kutoka divisheni kwenda GPA.
Profesa Ndalichako amesema kuwa sababu walizozitoa baraza la mitihani nchini kuhusiana na kuhama mfumo wa utoaji matokeo ya mitihani kutoka divisheni kwenda GPA hazikuwa na msingi wowote na wala hapakuwa na ulazima wa kufanya hivyo.
Amesema katika siku saba alizozitoa kwa baraza hilo kutoa sababu za kuhama kutoka mfumo wa divisheni kwenda GPA baraza hilo limeshindwa kutoa sababu za msingi na badala yake limetoa maelezo tu ambayo hata hivyo nayo hayana msingi wowote.
"Baraza la mitihani (NECTA) acheni kucheza na elimu ya watanzania kwa kuwa lengo la wizara ya elimu ni kutoa elimu bora kwa kila mtanzania tena elimu iliyo bora zaidi". Alisema Waziri Ndalichako
Mbali na hilo Profesa Ndalichako ameliagiza baraza la taifa la mafunzo ya ufundi (NACTE) kuangalia upya viwango vyao vya ufaulu wanavyoviweka kutokana na wengi wa vijana wanaohitimu katika vyuo vya ufundi kutokidhi vigezo katika soko la ajira.