Rais ameyasema hayo wakati akihutubia watanzania kupitia vyombo vya habari katika mkutano ulioandaliwa na wazee wa jiji la Dar es salaam.
"Nchi hii ina majipu kila mahali kuna watu hawana shida ya pesa kabisa , ni watu wachache na fedha hizo walizipata visivyo halali na watanzania wengi wakabakia masikini wa kutupwa.
Natoa mifano michache tuu wilayani Bariadi kuna barabara imejengwa kwa kipande cha kilomita moja tuu ikagharimu bilioni moja zikajengwa kilomita 4.5 zikatumika bilioni 9.2 na wakuu wote wa serikali wapo.
''Mimi nimefanya kazi serikalini kwa miaka 20 pamoja na kuwa waziri wa ujenzi sijawahi kujenga barabara kilomita 4 kwa pesa kama hiyo, fedha ingetosha kujenga kilomita 20 za lami''
Rais ameongeza kuwa pia suala la bandarini ni aibu kwa miaka 5 mafuta yanayopitia bandarini yalikuwa haya pimwi hivyo serikali imepoteza mapato mengi sana kwa ukwepaji wa kodi.
''Nawasihi watanzania wenzangu mkiniona natumbua majipu au mawaziri wangu wanafanya hivyo waungeni mkono nchi hii kila kona ni majipu ni lazima tuyatumbue ili pesa zipatikanne zikahudumie wananchi wa hali ya chini'' Amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wao wazee wa mkoa wa Dar es salaam kupitia kwa mwenyekiti wao Mzee Hemed Mkali amemhakikishia Rais Dkt John Magufuli kwamba wazee wote wanamuunga mkonno kwa dhati kwa kasi yake ya utendaji serikalini.
Mzee Hemed ameyasema hayo wakati akisoma hotuba yao ambayo waliiandaa kwa ajili ya kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa aliyoyafanya akiwa madarakani kwa siku 100.
Sisi wazee tunaona na tunathamini sana unayoyafanya maarufu kama kutumbua majipu tunakuomba endelea hivyo hivyo mradi usimuonee mtu ili utendaji wa wafanyakazi wa serikali uzidi kuimarika siku hadi siku.
Mzee huyo ametaja baadhi ya mafanikio ambayo yamepatikana tangu kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano kuwa ni pamoja na kuokoa bilioni 7 za kusafiria viongozi mbalimbali, trilioni 1.3 kutoka bandarini, bilioni 4 ambazo zilikuwa zitumike katika sherehe za uhuru pamoja na kushughulikia watendaji wazembe serikalini na kuimarisha hospitali ya muhimbili jijini Dar es salaam.
Aidha mzee Hemed amemtaka Rais Magufuli kutokata tamaa au kulegeza kamba kwani watanzania wanamwamini na wana matarajio makubwa na serikali yake katika kuwakomboa watanzania.





