Wednesday , 31st Oct , 2018

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri amesema wakuu wake wa Wilaya wameanzisha utaratibu maalum wa kuwakagua wageni wanaoingia mkoani humo kwa lengo la kutokomeza biashara haramu ikiwemo ya ukahaba, na madawa ya kulevya.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Agrey Mwanri.

Mwanri ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na www.eatv.tv jijini Dar es salaam alipokuwa akiwasilisha mpango wa mkoa wake wa kuandaa jukwaa maalum litakalohusu uwekezaji katika mkoa huo.

Katika maelezo yake, aligusia suala la biashara ya ukahaba mkoani humo ambapo amesema kuwa wengi miongoni mwa watu hao wamekuwa wakitokea mikoa mingine hasa Dar es salmaa na kuingia mkoani humo.

Ukienda kwenye nyumba za wageni za Tabora, utashangaa kumuona mtu anatakata tu lakini hujui biashara anayofanya, nimewagiza wakuu wangu wa wilaya wakipita watu ambao hawajulikani wakaguliwe kazi gani wanafanya", amesema Mwanri.

Kuhusiana na suala la elimu Agrey Mwanri amesema mpango wake ni kuhakikisha kila nyumba ya mkazi wa Tabora inafanikiwa kutoa muhitimu wa elimu ya Chuo Kikuu.

Mwanri amesema “ukitaka wananchi wako wawe  na vifaa waelemishe watu wako, usiwadharau, tunalofanya na mpango tulionao ni kutoa wahitimu wa chuo kikuu katika kila nyumba ya mkazi wa  Tabora, hata bibi kizee mwenye miaka 80 atapata degree (Shahada ya kwanza) lakini miaka 30 ijayo hatakuwepo ndio maana tunawekeza kwa watoto.”