Thursday , 15th Jan , 2015

MKAZI wa mtaa wa Kitwana kata ya Busoka wilayani Kahama mkoani Shinyanga Regina  Shija (55) ameuawa kwa kukatwakatwa mapanga kichwani  na watu wasiojulikana kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa Kimapenzi.

Afisa mtendaji wa Mtaa huo, Bw. Rafael Jumanne ameiambia amesema kuwa tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 5.00 usiku ambao watu wasiofahamika walivamia nyumbani kwa  Regina akiwa  anajiandaa kulala na wajukuu wake wawili.

Amesema baada ya watu hao ambao idadi yao haijafahamika, kuvamia nyumbani hapo walianza kumkatakata mapanga mama huyo kichwani na  mkono wa kulia hali iliyosababisha kuvuja damu kwa wingi baadaye kufariki dunia.

Afisa Mtendaji huyo amedai kuwa chanzo cha  mauji hayo bado haijafahamika ingawa yanahusishwa na wivu  wa kimapenzi na kwamba   jeshi la Polisi lilifika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu huyo na kuupeleka kuuhifadhi katika chumba cha kuhifadhia maiti kwenye hospitali ya wilaya ya Kahama.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga Bw. Justus Kamugisha  amethibitisha kutokea kwa tukio  hilo ambapo amesema hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na kuwa jeshi hilo linaendelea na upelelezi huku akiwaomba wananchi kulisaidia kwa kutoa taarifa za siri zitakazoweza kulisaidia kuwabaini wahusika na hatimaye kuwakamata na kuwafikisha  katika vyombo vya sheria.