Tuesday , 30th Dec , 2014

Waziri wa Uchukuzi Mh Dk Harrison Mwakyembe ametoa siku 14 kwa kampuni ya AMI ambayo inajisughulisha na utunzaji wa mizigo kutoka bandarini maarufu kama bandari kavu kuhakikisha kuwa inalipa kontena la mteja ambalo lilipotea.

Waziri wa Uchukuzi Mh Dk Harrison Mwakyembe ametoa siku 14 kwa kampuni ya AMI ambayo inajisughulisha na utunzaji wa mizigo kutoka bandarini maarufu kama bandari kavu kuhakikisha kuwa inalipa kontena la mteja ambalo lilipotea katika himaya yao na kama hawatafanya hivyo hawataruhusiwa kujishughulisha na kazi yoyote katika bandari ya Dar es salaam.

Mh waziri ametoa agizo hilo alipokutana na watendaji wa mamlaka ya bandari pamoja na makampuni mbalimbali ambayo yanafanya kazi na bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kujua changamoto mbalimbali ambazo wanakumbana katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumzia agizo hilo meneja uendeshaji wa AMI Bw Mbonea Bohela amesema wamemtaka mlalamikaji kupeleka nyaraka za mzigo wake ili jambo hilo lishughulikiwe lakini mpaka sasa hivi hajafanya hivyo.

Mwakyembe ameuagiza uongozi wa Kampuni ya Kupakua na Kupakia Makontena Bandarini (TICS) kufika ofisini kwake kesho ili kutoa ufafanuzi kuhusiana na madai ya kukiuka masharti ya utoaji wa huduma.

Waziri Mwakyembe ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam leo, katika mkutano wake na wadau wa sekta ya uchukuzi wakiwemo wawakilishi wa wafanyabiashara kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo amezitaja gharama hizo kuwa ni viwango vya juu vya thamani ya kubadilishia fedha za kigeni vinavyotozwa na kampuni hiyo tofauti na viwango vinavyotolewa na benki kuu ya Tanzania.

Aidha Dkt Mwakyembe amewataka watoa huduma wote ndani na nje ya bandari hiyo kuhakikisha wanafuata utarataibu wa kisheria uliowekwa ili kusaidia kutoa huduma bora kwa watumiaji wa bandari hiyo

Wakitoa malalamiko yao wafanyabishara wa Congo ambao wanatumia bandari hiyo wamesema muda wanaopewa kurudisha kontena wakishachukua mzigo bandarini ni mdogo na hivyo wanaomba muda uongezwe.

Kwa upande chama cha mawakala wa forodha TAFFA wamelalamikia kitendo cha kuwekwa kwa masharti magumu katika upatikanaji wa leseni za forodha sambamba na kutozwa fedha za uhifadhi wa mizigo katika bandari kavu hata kama mzigo bado haujafika katika bandari hizo.