Wednesday , 8th Apr , 2015

Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha usiku wa Jana imeharibu zaidi ya hekari Hamsini za mazao mbalimbali katika Kijiji cha Mungere Wilayani Monduli Mkoani Arusha na kusababisha hasara kubwa kwa wakazi wa eneo hilo.

Pichani ni athari na madhara yaliyosababishwa na mvua ambayo imenyesha usiku wa kuamkia juzi, wilayani Karatu na Monduli mkoani Arusha,

Wakizungumza na kituo hiki katika eneo la Mungere lililofikwa na maafa hayo, wanakijiji walioathiriwa na mvua pamoja na upepo mkali, wamesema maafa hayo yamewarudisha nyuma kiuchumi, kutokana na wengi wao kujikita katika kilimo cha migomba, baada ya mwaka 2009 kukumbwa na janga jingine la mifugo yao kufa kutokana na ukame.

Mmoja wa wakulima katika Kijiji cha Mungere, Zephania Maliki ambaye amepoteza takribani hekari mbili za migomba, amesema alitegemea kuvuna migomba yake mwishoni mwa mwezi April, lakini kufuatia maafa hayo mazao aliyokuwa akiyategemea kwaajili ya chakula na biashara yote yamesombwa na maji, huku akiomba msaada wa dharura kukabiliana na janga la njaa linalotazamiwa kukumba eneo hilo.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Esilalei Naturi Leiyo amesema athari ya mvua hizo ni kubwa kutokana na kaya nyingi kukosa chakula na mahitaji mengine na kuhamasisha wananchi kupanda miti kandokando ya mashamba.

Tathmini ya hasara iliyopatikana kutokana na maafa hayo bado haijafahamika mara moja huku wakazi wa eneo hilo ambalo ni ukanda wa bonde la ufa likipakana pia na hifadhi ya wanyama ya Manyara wakibainisha kwamba hawakuwahi kushuhudia mvua kubwa iliyoambatana na upepo katika kipindi chote kama ilivyokuwa hivi sasa.