Thursday , 12th Nov , 2015

Wakulima wadogo nchini wameiomba serikali kuwaandaa katika kuingia kwenye ushindani wa soko la kimataifa ili kuwawezesha kushindana na nchi nyingine katika ubora wa bidhaa wanazozalisha .

Mwenyekiti wa Mviwata Veronika Sophu akizungumza na waandishi wa habari wanaoandika habari za wakulima (kulia) ni Mkurugenzi wa Mviwata Stephen Ruvuga.

Wakizungumza katika mdahalo wa kuchangia wakulima wadogo kuhusiana na masuala ya biashara ya kilimo cha kimataifa na usalama wa chakula duniani ulioandaliwa na mtandao wa vikundi vya wakulima wadogo Tanzania(MVIWATA) wakulima hao wamesema hawajaandaliwa kuzalisha mazao bora ya kilimo yanayokubalika kwenye soko la kimataifa na katika usafirishaji wa mazao hayo katika kiwango bora.

Kwa upande wake afisa sera na utetezi MVIWATA taifa Bw. Thomas Laiser amesema kwa kuwa kuna mkutano wa mawaziri wa nchi wanachama wa shirika la biashara duniani (WTO) unaotarajia kufanyika mjini Nairobi nchini Kenya na kwamba watatumia fursa ya mdahalo huo kuweza kutoa mapendekezo yao.

Akitoa ufafanuzi kuhusu Tanzania kujiunga katika Shirika la Biashara Dunia (WTO) mwakilishi wa wizara ya viwanda na biashara bw Ernest Elias amewashauri wakulima kujiunga kwenye vikundi mbalimbali vya wakulima na biashara ili kuweza kupata fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali.