Sunday , 14th Sep , 2014

Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Tanzania RED CROSS kimesema kuwa kinaendelea kujenga vituo mbalimbali vya kuwahifadhi watu wenye albinism katika mikoa ya Simiyu, Geita na Tabora ili kuwaokoa na wimbi la kufanyiwa vitendo vya ukatili.

Akiongea leo jijini Dar es Salaam Afisa Uhusiano wa RED CROSS Tanzania Raymond Kayombo amesema wao kama sehemu ya kutoa misaada ya uokoaji kwa watu wanaendelea na jitihada mbalimbali za kuwaepusha watu wenye albinism na hatari inayoweza kuwapata.

Kwa mujibu wa Raymond kujengwa kwa vituo hivyo ni moja kati ya njia za kuhakikisha usalama wa watu wenye Albinism ambao kwa sasa wanawindwa na kufanyiwa ukatili kutokana na maeneo wanayoishi wengi wao kuwa duni na yasiyokuwa na ulinzi.

Wakati huo huo, Zaidi ya washiriki mia mbili wanatarajia kushiriki mashindano ya riadha za Serengeti Marathon, yatakazofanyika ndani ya mbuga ya wanyanya ya Serengeti mkoa wa Mara huku lengo lake kuu likiwa ni kuinua sekta ya utalii kupitia michezo.

Mbio hizo zimeandaliwa na taasisi ya michezo ya Serengeti Sports Centre ambapo kwa mujibu wa Mkurugenzi wake Mkuu Bi. Maggie Mlengeya, mashindano hayo yatatumika pia kuhamamisha jamii kuendeleza mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa watu wenye ulemavu wa ngozi maarufu kama albino.

Bi. Maggie Mlengeya ameongeza kuwa mashindano hayo yatahusisha mbio zenye umbali wa kilomita 42, kilomita 21 na kilomita tano ambazo zitafanyika ndani ya mbuga ya wanyama ya Serengeti.