Kushoto ni gari ya Msaidizi wa IGP,Ernest Mangu, Ndugu Gerlad Ryoba picha Ndogo ( Kulia)baada ya kutolewa eneo la tukio
Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Dodoma, kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma, David Misime amesema kuwa tukio hilo lilitokea januari 3 mwaka huu majira ya saa 3 usiku ambapo miongoni mwa watu waliofariki ni familia ya mkaguzi wa polisi ambaye pia ni Msaidizi wa Inspekta jenerali wa polisi, Gerald Ryoba iliyokuwa ikitokea Mkoani Geita kuelekea mkoani Dar es Salaam.
Kamanda Misime amesema kuwa katika ajali hiyo Ryoba alikufa yeye pamoja na mkewe aliyemtaja kwa jina la Fidea John Kiondo ambaye alikuwa ni mwalimu wa shule ya msingi Wilayani Temeke Mkoani Dar es Salaam, pamoja na watoto wao wawili wa kiume.
Pia Kamanda Misime amesema kuwa katika kusaka miili ya marehemu hao walikuta miili mingine ya watu wawili akiwemo mtu mmoja aliefahamika kwa jina la ludege ambae ni Afisa Mifugo pamoja na mwili mwingine ambao haujafahamika huku akiongeza kuwa wataendelea kukagua mto huo ili kubaini kama kuna watu zaidi waliofariki kutokana na maji hayo.
Aidha kamanda Misime ametoa wito kwa madereva kuwa makini wanapokuwa wanaendesha hasa kwenye maeneo yenye maji mengi ili kuepusha maafa.
Kaimu mganga mfawidhi wa hospital ya rufaa ya mkoa wa Dodoma, Dk, Ibenzi Ernest amethibitisha kupokea maiti sita za watu waliokufa kwenye ajali hiyo ya maji mjini Kibaigwa