Wednesday , 18th Feb , 2015

Hekta zipatazo 17 ziliziomo ndani ya hifadhi ya taifa ya msitu wa Jozani kisiwani Zanzibar zimeteketea kwa moto ambao unasadikiwa umetokana na wavunaji haramu wa asali.

Moto huo umedhibitiwa na vikosi vya ulinzi na uokozi na wafanyakazi wa wizara ya kilimo kwa kushirikiana na wananchi kutokana na magari ya zimamoto kushindwa kufika ndani zaidi ya msitu ambapo hekta hizo 17 zimeathirika kati ya heta 5000 zilizopo katika msitu huo wa Jozani ambao pia ni maarufu kwa watalii.

Kutokana na moto huo makamu wa pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi alifika katika msitu huo na kujionea athari za moto huo uliozuka katika msitu wenye hadhi kubwa kwa Zanzibar kutokana na mazingira ya miti yake na wanyama adimu duniani.

Akizungumza na watendaji wa wizara balozi Seif mbali ya kuwapongeza wananchi na askari kwa kudhibiti moto huo amesema iko haja ya hatua za makusudi kuchukuliwa dhidi ya wavunaji hao haramu ambao wamekuwa kero katka misitu.

Mapema katibu mkuu wizara ya kilimo Afan Othman alisema unyevunyevu uliopo kwenye eneo hilo nao umechangia kuepusha athari zaidi za kuenea kwa moto huo kwa kutoathiri miti mikubwa na msitu huo pia ni tegemezi kubwa kwa wakulima wa mpunga.

Naye mkuu wa kikosi cha zimamoto na uokozi wa mkoa wa kusini Unguja SSF Shaban Ramadhan Ali amesema bado kikosi kina uhaba mkubwa wa vifaa vya kisasa na magari yenye uwezo wakukabiliana na maafa ya aina hiyo

Hifadhi ya taifa ya msitu wa Jozani imekuwa maarufu kimataifa kutokana na maumbile yake ya kuwa na viumbe mchanganyiko wakiwemo wanyama adimu kama Kima Punju, Paa nunga, Nguruwe, Vipepeo na aina mchanganyiko ya ndege na miti mbalimbali.