Thursday , 10th Jul , 2014

Mbunge wa Musoma vijijini Nchini Tanzania, Mhe. Nimrod Mkono amesema wakati wa vijana kuongoza nchi bado haujafika ila wanahitaji kushirikiana na wazee katika kulijenga taifa kwa sasa.

Mbunge wa Musoma Vijijini Nimrod Mkono.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari Mkono amesema vijana walio katika ulingo wa siasa wana ndoto za kuchukua nafasi za juu za uongozi ikiwemo urais bila kufuata taratibu na ushauri kutoka kwa wazee.

Mhe. Mkono amesema majukumu ya kuongoza nchi yanahitaji busara na utulivu wa maamuzi katika uongozi hivyo kuwataka vijana wenye ndoto za kupata uongozi washiriakiane nao katika kulijenga taifa.

Kauli ya mkono imekuja siku chache baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Mahusiano na Uratibu ambaye pia ni mwanasiasa mkongwe Stephen Wassira kutoa kauli kama hiyo kwa madai kuwa Tanzania bado ina wazee wazalendo, wenye busara ya uongozi na wanaotambua matatizo na changamoto zinazoikabili nchi hivi sasa.

Malumbano kuhusu umri wa mgombea Urais yamekuja kufuatia aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba kudai kuwa Tanzania hivi sasa inahitaji viongozi vijana wenye nguvu na mawazo mapya ya namna ya kukabiliana na matatizo ya kijamii na kiuchumi.