Huu ni mnara wa kuongozea ndege katika kiwanja hicho cha Songwe katika Mkoa Mpya wa Songwe,
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro amesema hayo alipotoa taarifa ya kuugawa mkoa wa Mbeya na kuanzisha mkoa mpya wa Songwe kwenye Kikao cha ushauri cha mkoa wa Mbeya(RCC) kilichohudhuriwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo wanaotoka katika halmashauri zinazounda mkoa mpya wa Songwe.
Kandoro amesema uamuzi wa kutumia ofisi ya wilaya ya Mbozi kuwa makao makuu ya mkoa mpya wa Songwe yamefikiwa maada ya majadiliano ya pamoja kati ya ofisi yake na ofisi za wakuu wa wilaya za Mbozi na Momba sambamba na ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi.
Mkoa mpya wa Songwe utaundwa na wilaya za Mbozi,Ileje, na Momba na wilaya mpya ya Songwe.Utakuwa na halmashauri za Ileje,Momba na Mbozi,halmashauri ya mji wa Tunduma na halmashauri mpya ya Songwe inayotarajiwa kuanzishwa
Amesema jengo la mkuu wa wilaya ya Mbozi litatumika kwa shughuli za sekretarieti ya mkoa lakini pia ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo itaendelea kutumia sehemu ya majengo kwaajili ya ofisi.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi atahamia kwenye majengo ya halmashauri yaliyopo jirani na ofisi mkuu wa wilaya hiyo hivyo maandalizi ya utambuzi wa ofisi kwaajili ya ofisi za mkoa mpya wa Songwe yamekamilika.
Kandoro amesema kuhusu nyumba ya kuishi mkuu wa mkoa na Katibu Tawala wa mkoa,ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mbeya imependekeza kuwa mkuu wa mkoa huo mpya atatumia nyumba ya sasa ya mkuu wa wilaya ya Mbozi ambayo itatumika pia kama Ikulu ndogo ya mkoa huo.
Katibu tawala wa mkoa huo atatumia nyumba ya sasa ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ambapo mkuu wa wilaya ya mbozi atahamia kwenye nyumba ya mhandisi wa ujenzi wa halmashauri hiyo huku mkurugenzi akihamia kwenye nyumba ya Mtunza hazina wa halmashauri.