Monday , 1st Dec , 2014

SERIKALI imetakiwa kufuatilia pesa zinazotolewa kwaajili ya wafanyakazi walio na maambukizi ya VVU ili kuwafikia walengwa ambao imewalenga kuwasaidia na kufikia malengo ya kupunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI.

Mwenyekiti Mtendaji Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania, (Tacaids), Fatuma Mrisho

Akizungumza katika kongamano la tathimini ya UKIMWI mkoani Njombe, Mwenyekiti wa waalimu wanao ishi na virusi vya UKIMWI Tanzania, Mwalimu Heleni Masawa, amesema kuwa serikali imekuwa ikitoa pesa kwa waalimu wanao ishi na virusi vya UKIMWI na haziwafikii walengwa.

Amesema kuwa TAMISEMI imekuwa ikitoa pesa kwa waalimu hapa nchini wanao ishi na virusi vya UKIMWI kwaajili ya kujikimu lakini zimekuwa zikikwama katika halmashauri, na kuto wafikia walengwa.

Aidha Mwenyekiti Mtendaji Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, (TACAIDS), Fatuma Mrisho amesema kuwa serikali imekuwa ikitoa pesa kwaajili jitihada ya kudhibiti UKIMWI hapa nchini kulingana na umbali wa eneo na ukubwa wa tatizo katika eneo husika.

Amesema kuwa wananchi wa Njombe wasiwe na wasiwasi na serikali kwa mkoa wa Njombe inatoa pesa nyingi kuliko mahali popote hapa nchini katika jitihada za kudhibiti UKIMWI kwa kutoa elimu, kinga na kusogeza huduma kwa jamii.