Tuesday , 8th Dec , 2015

Jumla ya sh. 675,436,159 zimetumika kwa ajili ya kuzilipa kaya 17,162 zilizopo wilayani sengerema katika mkoa wa mwanza kwa ajili ya kuzikwamua kuondokana na wimbi la umaskini.

Moja ya Nyumba zilizopo vijijini ambazo Kaya yake inatakia kupewa pesa za TASAF

Mratibu wa mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) wilayani humo, Rehema Simeon, akizungumza wakati wa kuzikabidhi kaya maskini za vijiji tisa wilayani humo, amesema lengo la mfuko huo ni kuwaondolea umaskini wananchi hao.

Amesema vipo vijiji 106 kati ya 153 ambavyo wananchi wake wapo katika malengo ya kuondolewa umaskini na tasaf, wamemaliza kaya za vijiji tisa kwa awamu ya tatu baada ya kuanza julai mwaka huu na kukamilika desemba mwaka huu.

Amevitaja vijiji ambavyo baadhi ya kaya zilikabidhiwa pesa kwa ajili ya kujikwamua na umaskini ni Mnadani, Mtakuja, Kizugwangoma, Kanyamwanza, Butonga road, Sima, Isungang’holo, Ishinshangholo na Ilyamchele.

Simeon amesema walengwa waliondolewa umaskini kwa kupatiwa pesa za mtaji wamekuwa wakipatiwa kati ya Sh. 20,000 hadi 78,000 kwa kila kaya hususani zikiwalenga akinamama ambao ni wasimamizi wakuu wa familia.

Hata hivyo, amesema changamoto wanayokabiliana nayo ni pale wanapokuta kaya imehama ama kufariki hivyo wenyeviti hudai kutaka kuachiwa pesa kwa makusudi ya kuzipatia familia ya kaya husika.

Naye kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Sengerema, Vincent Bushaija, amewataka walengwa wa kaya zilizopata pesa hizo, kuweza kujiwekea malengo ya kuzitumia na kupata mabadiliko ya kimaisha.