Wednesday , 23rd Aug , 2017

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, amepiga marufuku wanafunzi kuchangishwa michango mashuleni bila kufuata utaratibu baada ya serikali kupiga marufuku michango ya aina yoyote inayofanywa na walimu.

Uchangishwaji huo wa michango umesitishwa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kupata taarifa kuwa shule ya Chadulu iliyopo Manispaa ya Dodoma yenye wanafunzi zaidi ya mia sita kuendelea kuwachangisha wazazi wenye watoto wanaosoma shule hiyo michango ya maji, afya na mitihani zaidi ya shilingi elfu sita kwa kila mwanafunzi.

"Naombeni michango yote hiyo muwarudishie wazazi kuanzia shilingi 200 ya mtihani, 5000 ya maji na hiyo michango ya Afya. Kama mnaona kuna sababu yoyote ya michango hiyo ni lazima tukae sisi wenyewe, mimi Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya mkurugenzi pamoja na nyie na baada ya hapo ndipo tuwashirikishe na wazazi. Maagizo ya kusitisha michango ni kwa shule zote za Dodoma," 

Bw. Rugimbana ameenda shuleni hapo kufuatia malalamiko ya baadhi ya wazazi kuwa licha ya serikali kupiga marufuku michango mashuleni yenye kero mbalimbali, lakini bado wanaendelea kuchangishwa na kuthibitishwa na Mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo Rhoda William.