Monday , 20th Apr , 2015

Hofu ya kutokea kwa mgomo mwingine wa nchi nzima wa madereva wa vyombo vya moto imetanda kutokana na madai ya serikali kushindwa kutimiza ahadi ya kukutana na viongozi wa muungano wa vyama vya madereva.

Kuna kila dalili ya kutokea kwa mgomo mwingine wa nchi nzima wa madereva wa vyombo vya moto, kutokana na madai ya serikali kushindwa kutimiza ahadi ya kukutana na viongozi wa muungano wa vyama vya madereva, kama ilivyoahidi April kumi mwaka huu, siku ulipotokea mgomo wa kwanza wa madereva hao.

Hali hiyo imebainika jijini Dar es Salaam leo, wakati viongozi wa muungano wa vyama vya madereva nchini waliokutana kujadili yaliyojiri Jumamosi ya April 18 mwaka huu, siku ambayo serikali ilikuwa ikutane na madereva hao kwa lengo la kushughulikia kero zilizosababisha mgomo huo ikiwemo mazingira bora ya kazi kukutana hii leo kuzungumzia mkutano huo.

Akitoa majumuisho ya mkutano huo, Mwenyekiti wa Muungano wa Vyama vya Madereva, Clement Masanja amesema inasikitisha kuona serikali imeshindwa kuwajibika kukutana na uongozi wa madereva hao ambao pamoja na mambo mengine, madai yao ni pamoja na kujadili mbinu jumuishi za kukabiliana na wimbi la ajali nchini.