
Gari Maalum kwa ajili ya kuchimbia visima katika jimbo la Pangani
Akizungumza na EATV, Mh Aweso amesema mbali na kupata mashine ya kuchimba visima, pia wamepata trekta, ambapo mbali na kutatua tatizo la maji, pia vitasaidia katika kilimo.
"Tuliwaomba taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Islamic Help iliyopo pangani trekta na gari la uchimbaji visima waliandika mradi na tumefanikiwa kupata trekta ambayo ina mashine kabisa ya kuchimbia visima, kwahiyo tutatatua tatizo la maji pamoja na kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji".
Amesema jimbo la Pangani lenye wakazi wapatao 54,000 limekuwa katika shida kubwa ya maji kwa miaka mingi licha ya kuwa na Mto Pangani, na wakazi wake wamekuwa wakitaabika kutafuta maji kutoka umbali mrefu, hivyo ameona kuliko kusubiri utekeleza wa ahadi za serikali ambazo zinachukua muda mrefu, ameamua kufanya jitihada zake kwa kushirikisha wadau.
Jumaa Aweso, Mbunge wa Pangani
"Tatizo la maji litapungua kwa kiasi kikubwa, sisi lengo letu kubwa ni kutumia maji ya mto Pangani, lakini mpaka serikali ilete pesa ,siyo leo, kwahiyo tumeona tufanye jitihada hizi, ndugu zetu wa Islamic Help watuchimbie visima ili wananchi kwa kipindi hiki waweze kupunguza adha ya maji. Jimbo langu lina wakazi takribani 54,000 ndiyo maana nabuni vitu vile vya msingi zaidi"
Kuhusu utaratibu wa kuanza kazi ya uchimbaji, amesema halmashauri ndiyo itakayohusika kupanga vijiji vya kuanzia, na ana uhakika jimbo zima litasahau kabisa tatizo la maji wakati wakisubiri fedha kutoka serikalini kwa ajili ya matumizi ya mto Pangani.