
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda (kulia) akiwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Akizungumza kwa www.eatv.tv James Mbatia, ili kufahamu kama angeitikia wito wa mkuu huyo wa mkoa Mbatia amesema anapenda maendeleo lakini kiongozi huyo alipaswa kufata taratibu kutoa mwaliko kwa viongozi hao.
“Yaani kweli mimi Mbatia nialikwe na Mkuu wa Mkoa (Makonda) kupitia vyombo vya habari sio sawa kabisa, hatukatai maendeleo lakini alipaswa kufata taratibu kabla za kunialika kwa kunitumia barua sio kutumia vyombo vya habari. ”, amesema Mbatia.
Kwa upande, wake Mkurugenzi wa Mambo ya Nje,Itikadi na Uenezi kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Mrema, amesema kama chama hawako tayari kupokea mwaliko uliotolewa kwenye vyombo vya habari, bali afate sheria rasmi na taratibu za serikali katika kuwaalika viongozi.
“Yeye kama kiongozi anajua taratibu za kuwasiliana na viongozi,tukipokea mwaliko rasmi tutasema, na sisi ni watu ambao tulikwisha sema hatuna shida ya kushiriki kwenye shuguli mbalimbali, hawezi kualika viongozi wetu kupitia vyombo vya habari,afuate utaratibu wa kiserikali”, amesema Mrema.
Naye Katibu wa Sera na Utafiti kupitia Chama Cha Wazalendo (ACT), Kweweta Idris, amesema ni lazima kufatwa kwa sheria katika kuwaalika viongozi nasio kwa tamko linatolewa kwa waandishi wa habari.
“Chama kama taasisi hatuwezi kupokea mwaliko kupitia vyombo vya habari, au mitandao ya kijamii nilazima tupate mwaliko rasmi kupitia barua au mwakilishi wa kutoka serikalini”, amesema Kweweta.
Mapema jana katika mkutano wake za kifedha Makonda aliwaalika baadhi ya wabunge wa Upinzani ili kuhudhuria tukio hilo ambalo linatajwa kupunguza adha ya foleni kwa watumiaji wa barabara ya Mandela a Nyerere na kusaidia kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 400.
“Ningependa kuona viongozi wa vyama vyote waje, akiwemo Mbatia, Mbowe, Zitto Kabwe na Halima Mdee wasisusie kama ilivyo mambo ya uchaguzi, nawaalika vyama vyote vya siasa mimi nitakuwa mwenyeji wao na tutawawekea viti ” alisema Makonda