Meneja Miradi na Biashara wa Soko la Hisa la Dar es Salaam - DSE, Patrick Mususa
Meneja Miradi na Biashara wa soko hilo Bw. Patrick Mususa amesema katika kipindi hicho idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa nayo imepanda kwa zaidi ya mara tatu kutoka hisa laki sita na sitini na tano elfu hadi hisa milioni mbili na laki nne.
“Tumeona kuwa katika kipindi cha juma moja lililopita mauzo yameongezeka sokoni na hali ya biashara kwa ujumla ni nzuri,” amesema Mususa na kuongeza kuwa hii inatokana na hatua kadhaa zinazochukuliwa na mdhibiti yaani DSE kuhakikisha wauzaji na wanunuzi wa hisa wanapata faida kulingana na uwekezaji wao.
Kwa mujibu wa Afisa huyo wa DSE, viashiria vya soko vimeonyesha kuwa sekta ya viwanda ndiyo inayoongoza kwa kufanya vizuri ikifuatiwa na sekta ya huduma za kibenki na kifedha huku sekta ya biashara ikishika nafasi ya mwisho.
Ameongeza kuwa hata mtaji wa soko nao umeongezeka kwa asilimia 2.5 na kufikia fedha za Tanzania shilingi trilioni 21.8 kutoka shilingi 21.2 huku ukubwa wa mtaji wa makampuni ya ndani ukibakia ule ule wa shilingi trilioni nane nukta tatu.