Mwenyekiti wa Chama cha Utabibu wa Dawa Asili nchini Tanzania (ATME) Bw. Simba Abdulrahman Simba.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, mwenyekiti wa chama hicho Bw. Simba Abdulrahman Simba amesema kimsingi pendekezo la sasa la kwamba rais awe na makamu wake watatu litaongeza mpasuko baina ya Watanzania sambamba na kuongeza gharama za kila siku za kuiendesha serikali.
Chama hicho kimependekeza kuwepo kwa nafasi ya rais na makamu wake wawili ambapo iwapo rais atatoka upande mmoja wa muungano, basi makamu wa kwanza wa rais atatoka upande mwingine huku makamu wa pili wa rais akiwa ni mtu anayetokea upande ambako rais wa Jamhuri ya Muungano anatokea.
Kwa mujibu wa Simba, hatua hiyo itasaidia ujenzi wa serikali yenye sura ya umoja wa kitaifa kwani mbali ya kuwa na mchanganyiko na uwakilishi kutoka pande zote za muungano; itasaidia pia kujumuisha uwakilishi wa vyama vya upinzani kwani wao wanapendekeza nafasi ya makamu wa pili wa rais iwe ya kiongozi kutoka chama kilichoshika nafasi ya pili katika uchaguzi mkuu.
Aidha, katika hatua nyingine, chama hicho kimeelezea kuridhishwa na jinsi mwanasiasa mkongwe mzee Kingune Ngombare Mwiru alivyoiwakilisha sekta ya tiba asili nchini na kutoa angalizo kuwa masuala ya tiba asili na huduma za afya kwa ujumla, yatamkwe ndani ya katiba ili yatekelezwe kwa ufanisi pasipo kutegemea utashi wa kiongozi aliyepo madarakani kwa wakati husika.