Thursday , 3rd Apr , 2014

Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam nchini Tanzania imetangaza rasmi kwamba inakusudia kukifunga kituo cha daladala cha Mwenge na kituo Kikuu cha mabasi cha Ubungo, na nafasi yake kuchukuliwa na kituo cha Makumbusho na kituo kipya cha Sinza.

Msemaji wa manispaa hiyo Bw. Sebastian Mhowera, ameyasema hayo leo katika mahojiano na East Africa Radio iliyotaka kufahamu kuhusu zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika maeneo yasiyo rasmi ikiwemo kwenye vituo vya mabasi na pembezoni mwa barabara.

Bw. Mhowera amefafanua kuwa kukamilika kwa vituo hivyo kutamaliza tatizo la wamachinga kuvamia vituo vya daladala ambapo pia amewataka viongozi wa serikali za mtaa na kata, kuhakikisha zoezi la kuweka mitaa yao linakuwa endelevu kwa kuhakikisha biashara zote zinafanywa katika maeneo rasmi.