Wednesday , 22nd Oct , 2014

Mama na mtoto wamefariki dunia baada ya kula chakula kinachosadikiwa kuwa na sumu katika kijiji cha Miranda tarafa ya Nshamba wilayani Muleba mkoani Kagera huku watoto wake wengine wanne wakiwa hospitalini wakipatiwa matibabu.

Kamanda wa polisi mkoani Kagera, Henry Mwaibambe, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja waliopoteza maisha kwa madai ya kula ugali wa muhogo wenye sumu kuwa ni Oliva Wilson miaka 42 na Nemilius Wilson miaka mitano.

Amesema watoto wengine wanne wa mama huyo Avira Wilson miaka 10, Frolida na Frola Wilson mapacha wenye miaka saba na Scarion Wilson miaka miwili, wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Rubya.

Kamanda Mwaibambe amesema unga wanaosadikiwa kutumiwa kwa ugali na familia hiyo, umekusanywa na kupelekwa kwa mkemia mkuu wa serikali kwa ajili ya vipimo ili kubaini kama ulikuwa na sumu ya aina gani.

Wakati huo huo, idadi ya akina mama wajawazito wanaokufa wakati wa kujifungua nchini Tanzania bado ipo juu ambapo takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa akina mama 454 hufariki dunia kati ya vizazi hai laki moja, huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni huduma duni za afya ya uzazi.

Mkuu wa Kitengo cha bidhaa, Uchuuzi na Mikakati wa Benki ya Barclays nchini Tanzania Bw. Mussa Kitoi, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati benki hiyo ilipozungumzia mpango wa kukusanya pesa kwa ajili ya kugharamia huduma za afya ya mama na mtoto, kupitia matembezi ya hisani yajulikanayo kama Step Ahead.

Kwa mujibu wa Kitoi, benki hiyo imeguswa na ukubwa wa tatizo la vifo vya akina mama wajawazito na kupitia matembezi hayo, jumla ya fedha za Tanzania shilingi milioni 200 zinatarajiwa kukusanywa na kukabidhiwa kwa taasisi za CCBRT na AMREF ambazo kwa sasa zinaratibu mpango wa mafunzo ya wakunga na huduma za afya ya uzazi.