Sunday , 10th Jun , 2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini kutowatumia watu tofauti nje ya taasisi zao kwa ajili ya kuwasemea kwani wanaweza kuwachonganisha na serikali yao.

Mh. Majaliwa ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na viongozi na wananchi wa Mkoa wa Mwanza baada ya kushirikiana nao katika futari aliyowaandalia, shughuli ambayo  ilihudhuriwa na waumini wa dini mbalimbali.

Majaliwa amesema kuwa serikali haiongozwi kwa misingi ya kidini bali imeziachia taasisi za kidini zifanye kazi kwa kuzingatia Katiba , Sheria za nchi na malengo yaliyokusudiwa katika uanzishwaji wake.

Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wake wanaishi kwa amani na utulivu, jambo litakalowawezesha kufanya shughuli zao kikamilifu, hivyo wasikubali kuchonganishwa kwa misingi yoyote.

"Nawaasa viongozi wa dini msikubali kutumia makundi mengine nje ya taasisi zenu kwa ajili ya kuwazungumzia masuala yenu kwa sababu watawachonganisha na Serikali ambayo haipo kwa ajili ya kugombana na taasisi yoyote,"amesisitiza.

Ameongeza kuwa jukumu kubwa la taasisi za kidini ni kuhakikisha wanawalinda waumini wao pamoja na kuwaongoza kwa kuwapa mafundisho mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu, ambayo yatawawezesha kuishi kwa amani.

Majaliwa amesisitiza kuwa amani na utulivu pamoja na mshikamano walionao wananchi umesababisha Tanzania kupata heshima kubwa dunia kote, hivyo ni vema kila mwananchi ahakikishe suala la kudumisha amani linapewa kipaumbele.