Wednesday , 6th Jul , 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo ameongoza mamia ya waumini wa dini ya kiislamu katika swala ya Eid el Fitri iliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.

Akitoa salamu za serikali Waziri Mkuu Majaliwa amekemea tabia ya madereva nchini kufanya mchezo na maisha ya watu barabarani jambo ambalo limezidi kuangamiza maisha ya nguvu kazi ya taifa.

Akitolea mfano ajali iliyotokea hivi karibuni katika mkoa wa Singida kwa mabasi mawili ya kampuni moja ya City Boy kugongana Waziri Mkuu ametumia wasaa huo kwa kuwaombea marehemu kwa dakika moja na baada ya hapo akasisitiza uwajibikaji wa mamlaka husika kwa madereva wanaohatarisha maisha ya watu.

''Tumeagiza vyombo vya dola kuendelea na kazi yao kwa kudhibiti madereva wazembe barabarani ili kuokoa maisha ya watu wasio na hatia wanaopotea kwa uzembe wa madereva'' Amesema Waziri Mkuu.

Aidha Waziri Mkuu ametumia nafasi hiyo pia kuwatakia waislamu nchini sherehe njema na kuhakikisha wanaendelea kutenda mema na kuhakikisha amani na mshikamano wa taifa unakuwepo.

''Siku hii ni siku ya kutembeleana ni siku ya ya kula pamoja na marafiki lakini pia kula na wasiojiweza, na kwa wale ambao wanaendelea kufunga tunawatakia sikukuu njema.

Hata hivyo Waziri Mkuu amewakumbusha waumini hao kwamba kama mtu alifunga na leo akafungua na kufanya madhambi Mwenyezi Mungu anakasirishwa sana na siku ya mwisho mtu wa aina hiyo atapata hukumu.